Psalms 51

Kuomba Msamaha

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi. Baada Ya Kukemewa Na Nabii Nathani Kwa Kuzini Na Bathsheba)


1 aEe Mungu, unihurumie,
kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,
kwa kadiri ya huruma yako kuu,
uyafute makosa yangu.

2 bUnioshe na uovu wangu wote
na unitakase dhambi yangu.


3 cKwa maana ninajua makosa yangu,
na dhambi yangu iko mbele yangu daima.

4 dDhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi
na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,
ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,
na kuwa na haki utoapo hukumu.

5 eHakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,
mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu.

6 fHakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni,
ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima.


7 gNioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi,
unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.

8 hUnipe kusikia furaha na shangwe,
mifupa uliyoiponda na ifurahi.

9 iUfiche uso wako usizitazame dhambi zangu,
na uufute uovu wangu wote.


10 jEe Mungu, uniumbie moyo safi,
uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.

11 kUsinitupe kutoka mbele zako
wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu.

12 lUnirudishie tena furaha ya wokovu wako,
unipe roho ya utii, ili initegemeze.


13 mNdipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako,
na wenye dhambi watakugeukia wewe.

14 nEe Mungu, Mungu uniokoaye,
niokoe na hatia ya kumwaga damu,
nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako.

15 oEe Bwana, fungua midomo yangu,
na kinywa changu kitatangaza sifa zako.

16 pWewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta,
hufurahii sadaka za kuteketezwa.

17 qBali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
moyo uliovunjika wenye toba,
Ee Mungu, hutaudharau.


18 rKwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi,
ukazijenge upya kuta za Yerusalemu.

19 Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki,
sadaka nzima za kuteketezwa za kukupendeza sana,
pia mafahali watatolewa
madhabahuni mwako.
Copyright information for SwhKC